Mazito yaibuka Zanzibar
WATU wasiojulikana wamevamia katika makazi ya watu eneo la Msumbiji mjini Unguja na kuvunja mabanda na msikiti.
Watu hao maarufu kama mazombi, walifanya uhalifu huo usiku wa kuamkia jana, ambapo walivamia eneo hilo wakiwa wamejifunika nyuso zao na soksi maalumu, huku wakiwa na silaha za jadi.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, aliliambia MTANZANIA kuwa watu hao walivamia eneo hilo saa 10 alfajiri.
Alisema watu hao baada ya kufika katika eneo hilo ambalo linadaiwa kukusanya mashabiki wa vyama vya upinzani, walianza kuvunja mabanda ya mafundi seremala.
“Lilikuwa kundi la watu, tena wote ni mazombi, wakiwa na silaha za moto pamoja na zile za kijadi kama mapanga, marungu, mikuki na mashoka.
“Wamefanya uharibifu mkubwa wa mali zetu yakiwamo mabanda ya mbao, msikiti wa mabati wa hapa Msumbiji ambao tumekuwa tukiutumia kama msikiti wa muda wakati huu wa kisasa ukiendelea kujengwa.
“Vurugu hizi wamefanya zimekuwa kubwa sana na uharibifu, huu kwa kweli ni uonevu wa hali ya juu, wameharibu mabanda karibu yote kama unavyoona na mengine ya biashara yaliyopo kando ya barabara hadi kufikia eneo la mabati,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazeti kwa kuhofia usalama wake.
MTANZANIA lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi lipo katika uchunguzi.
“Tumepata taarifa za tukio la kuvunja vibanda katika eneo la Msumbiji na Jeshi la Polisi tumeanza msako wa kuwabaini watu waliohusika na tukio hili, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kamanda Mukadam,
Dk. Shein na Uchaguzi
Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina sababu ya kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani hapa.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wana CCM na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kushirki uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Machi 20.
Kauli hiyo imekuja wiki moja baada ya Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), kupitia Kaimu Mwenyekiti wake, Dk. Twaha Taslima, kutangaza chama hicho kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio.
Dk. Shein aliyasema hayo jana mjini Unguja, alipokuwa akihutubia katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, ambapo aliwataka wanachama hao kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akisisitiza amani na utulivu visiwani humo.
“Sisi hatutasusa, tutashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi. Niwaombe nyote wanachama, kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili muichague CCM kwa kura nyingi,” alisema Dk. Shein.
Rais huyo wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, aliwataka wananchi pamoja na viongozi wa CCM kuendelea kushikamana pamoja ili waweze kuleta maendeleo ya kweli ndani ya chama hicho.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewahakikishia wananchi wote kwamba kutakuwa na ulinzi wa hali ya juu katika uchaguzi wa marudio.
“Nawasihi wananchi msiwe na wasiwasi, tutahakikisha ulinzi unaimarishwa ili muweze kupiga kura kwa amani na utulivu,” alisema Balozi Seif.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alimsifu Dk. Shein kwa kuwa kiongozi hodari na ambaye amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Hata hivyo aliwataka wananchama wa CCM kujipanga kwa ajili ya uchaguzi ili waweze kukipatia chama chao ushindi wa kishindo.
“Uchaguzi ni kujipanga, uchaguzi ni mikakati na uchaguzi ni mahesabu, kwahivyo niwaombe na nyinyi mzingatie haya,” alisema Kinana.
Sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM hufanyika kila mwaka nchini ambapo kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika mkoani Singida, Februari 6.
Visiwa vya Zanzibar vipo katika sintofahamu ya kisiasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alipotangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka jana.
Kutokana na hali hiyo, wiki iliyopita Baraza Kuu la Uongozi la CUF, kupitia Kaimu Mwenyekiti wake Dk. Taslima, walitangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio.
Kutokana na msimamo huo, mwishoni mwa wiki iliyopita mabalozi wa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) walitoa tamko la kusikitishwa na kitendo cha ZEC kutangaza tarehe ya kurudiwa uchaguzi na kumtaka Rais Dk. John Magufuli kutumia nafasi yake ya uongozi kutatua mtanziko wa kisiasa wa Zanzibar.
Taarifa ya pamoja iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mabalozi hao, pia inamtaka Rais Magufuli kuendeleza wito wake wa kuzitaka pande zote zitafute suluhu kwa amani.
Kutokana na sakata hilo, mabalozi hao wamelaani kitendo hicho wakisema kurudia uchaguzi kwa kigezo kuwa utaratibu ulikiukwa, kinawatia wasiwasi kwa kuwa tume hiyo haikutoa ushahidi wa ukiukwaji huo.
Mabalozi hao walisema katika tamko lao kuwa ZEC imerudia kauli yake ya kuwa uchaguzi ulikiuka taratibu licha ya waangalizi kutoka EU, Jumuiya za Afrika Mashariki, SADC, Marekani na Jumuiya ya Madola kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa ulikuwa uchaguzi huru na haki.
Taarifa hiyo iliyotumwa kwa ushirikiano wa mabalozi wa Uholanzi, Norway, Hispania, Italia, Ujerumani, Finland, Ufaransa, Sweden, Uswisi, Uingereza, Ireland na Marekani inasisitiza kuwa kitendo cha upande mmoja kuamua kurudia uchaguzi, kinaweza kuzidisha hofu na taharuki miongoni mwa Wazanzibari.
Chanzo: Gazeti la MTANZANIA
Labels:
habari
Post a Comment