vote
Featured Post Today
print this page
Latest Post

Askari aliyemuua Mwangosi atiwa hatiani



MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa, imemtia hatiani   Polisi, Pasficus Simon kwa   kumuua bila kukusudia, aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi.
Hukumu hiyo ilisomwa jana mahakamani hapo kwa zaidi ya saa tatu mbele ya Jaji   Paul Kihwelo.
Mwangosi aliuawa Septemba 2, 2012 katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi mkoani hapa, baada ya askari kuzuia mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Upande wa Jamhuri uliwasilisha  mahakamani mashahidi wanne ambako ushahidi wa shahidi wa kwanza, wa pili na wane, wote kwa pamoja ulishindwa kutoa vielelezo vya wazi dhidi ya mshtakiwa huyo kuwa aliuwa kwa kukusudia.
Jaji Kihwelo alisema jukumu la kuonyesha mshtakiwa alitenda kosa hilo ama la, lilikuwa la upande wa Jamhuri ambao walipaswa kuwasilisha ushahidi   ambao ungeweza kumtia hatiani mshtakiwa pasi na kuacha shaka ya aina yoyote.
Alisema mahakama inajiuliza juu ya ushahidi uliowasilishwa na shahidi namba moja, mbili na nne.
Jaji alisema  shahidi  namba tatu ambaye ni Mlinzi wa Amani, Flora  Mwolera ndiye aliyetoa ushahidi unaoweza kutumiwa na mahakama kufikia uamuzi.
Kwa mujibu wa ushahidi wa Flora ni kwamba mtuhumiwa alikiri kumuua   Mwangosi bila kukusudia na mahakama ilijiridhisha na ushahidi huo pasi na shaka yoyote hivyo ilimtia hatiani mshtakiwa kwa kosa hilo.
Alisema upande wa utetezi kupitia shahidi namba moja ambaye ni mtuhumiwa, kukana ungamo hilo kuwa alilitoa kwa mlinzi wa amani akiwa hayuko huru mahakamani, ilipingana na maelezo hayo kwa kuwa yangepaswa kupingwa kabla kesi haijafungwa.
“Lilikuwa ni jukumu la upande wa utetezi kuleta pingamizi  la kukataa ungamo hilo kabla ya kesi kufungwa kwa njia ya maandishi ama ya mdomo hivyo utetezi huo hauwezi kuzuia mahakama kumtia mtuhumiwa hatiani.
“Upande wa Jamhuri umeshidwa kuleta ushahidi unaojitosheleza bila ya kuacha shaka kuwa  mtuhumiwa alimuua Mwangosi kwa kukusudia.
“Hivyo mahakama itatumia ushahidi wa shahidi namba tatu
unaoonyesha mtuhumiwa amekuwa na hatia ya kuua bila kukusudia,”alisema Jaji.
Baada ya kutoa maelezo hayo Jaji Kihwelo,  alitoa nafasi kwa Wakili wa wa upande wa Jamhuri, Adolf Maganda, ambaye alidai mtuhumiwa huyo hana rekodi ya makosa ya aina hiyo.
Aliiomba mahakama kutumia kifungu namba 198 cha makosa ya adhabu kilichofanyiwa marekebidho mwaka 2002.
“Mheshimiwa Jaji ninaiomba mahakama yako tukufu impe adhabu mtuhumiwa, ikiwezekana kifungo cha maisha gerezani,” alisema Wakili Maganda.
Baada ya Wakili Maganda  kutoa maelezo yake,  Jaji Kihwelo alitoa nafasi kwa Wakili wa upande wa utetezi, Rwezaura Kaijage kuzungumza na mteja wake kwa muda mfupi kabla ya   kutolewa  adhabu.
Wakili Kaijage, alisema kwa kuwa mahakama imeshamtia hatiani mshtakiwa kwa kuona ameua bila kukusudia  na kwa kupitia maombi ya mshtakiwa kutaka apunguziwe adhabu.
“Mheshimiwa Jaji, mtuhumiwa ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 27 na bado taifa linamtegemea.
“Katika operesheni iliyofanyika Septemba 2, mwaka 2012 ambako ndipo maafa hayo yalipotokea hakwenda kwa idhini yake bali alikuwa akifanya hivyo kwa kuwa wao hufanya kazi
kwa amri.
“Silaha iliyotumika ilijifyatua kwa bahati mbaya, mtuhumiwa hakuwa na uwezo wa kuizuia kwa kuwa lilikuwa nje ya uwezo wake.
“Mshtakiwa ameshakaa mahabusu kwa miaka minne na katika kipindi hicho amekwishajutia kosa alilolitenda,” alidai Wakili Kaigaje.
Wakili huyo wa utetezi alisema     wazazi   wote wa mshitakiwa wamekwisha kufariki dunia hivyo ana jukumu la kuwalea wadogo zake watano walioachwa pamoja na mtoto wake mdogo mwenye umri wa miaka mitano.
Baada ya kusikiliza hoja hizo Jaji Kihwelo aliahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya kutoa adhabu kwa mshtakiwa aliyetiwa hatiani.
Chanzo: Gazeti la Mtanzania
0 comments

Mzee wa Upako: Lowasa ni tishio CCM

Anthon lusekelo

MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo, ameibuka na kuzungumzia uongozi wa Rais John Magufuli na sababu zilizochangia jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutawala Mkutano Mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliomalizika Dodoma mwishoni mwa wiki.
Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mchungaji Lusekelo, maarufu kama ‘Mzee wa upako’, alisema ilikuwa ni vigumu kumalizika   mkutano huo wa CCM pasipo kutaja jina la Lowassa kwa kuwa ndiye alikuwa tishio katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba mwaka jana.
“Lowassa ni tishio ….hivyo ilikuwa ni ngumu kukwepa kutaja jina lake katika mkutano huo maalumu wa CCM ambao Magufuli alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tano wa chama hicho,” alisema Lusekelo.
Katika mkutano mkuu huo, viongozi mbalimbali wa chama hicho walionekana kupagawa na kutaja jina la Lowassa kwa kumpiga vijembe kila walipokuwa wakizungumza.
Lowassa alijiengua CCM katika kipindi cha uteuzi baada ya jina lake kukatwa likiwa kwenye ngazi ya Kamati Kuu.
Alijiunga na Chadema na kuteuliwa kugombea urais akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kumpa wakati mgumu mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.
Lusekelo alisema kuondoka kwa Lowassa kulisababisha kutokea mpasuko wa fikra ndani na nje ya CCM, jambo lililosababisha kuondoka kwa makada wengi wa kawaida na waliokuwa na vyeo.
“Ndani ya CCM kulitokea makundi ambayo yaliibua mpasuko hivyo tutumie muda wa sasa kuyafukia ili kila mmoja aanze kuchapa kazi.
“Huu ni mwaka wa kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo hivyo tutumie muda huu kujenga utaifa na si kuendelea kupigana vijembe.
“Nasema hivyo kwa sababu naona hawa makada wanaorudi kwenye vyama vya awali kama Chadema na CCM wanaishia kupigana vijembe tu na kuendeleza majadiliano yasiyokuwa na msingi.
“Huu ni wakati wa kujenga umoja wetu kwa sababu amani ikitoweka itakuwa balaa kama ilivyo Sudan Kusini hivi sasa… na ninaamini nchi hiyo haitaweza kurejea tena kwenye amani hivi karibuni itakuwa kama Somalia. Naomba Watanzania tusifike huko,” alisema mchngaji huyo.
Alisema madaraka ni chanzo kikuu cha   vita katika nchi nyingi za Afrika, hivyo Tanzania inatakiwa kujifunza kutoka huko ili isiingie kwenye machafuko ya namna hiyo.
Pamoja na mambo mengine, alisifia uongozi wa Rais Magufuli akisema   wanaomwita kuwa ni dikteta uchwara hawajui maana yake.
“Watanzania wampe muda wa mwaka mmoja tu wataona mafanikio yake kwa sababu ni kiongozi mtekelezaji, kila kona ya nchi sasa kazi zinafanyika, ameijenga taswira nzuri ya Tanzania,” alisema.
Kiongozi huyo wa kiroho pia alizungumzia malalamiko ya wapinzani dhidi ya uongozi wa Rais Magufuli ikiwamo kupiga marufuku mikutano ya siasa.
Alisema hiyo inatokana na udhaifu uliopo kwenye Katiba ya mwaka 1977 inayotumika sasa.
“IGP anateuliwa na Rais, na Rais mwenyewe ndiye Amiri Jeshi Mkuu,  sasa hapo tutarajie nini lazima wamweshimu kwa kila kitu.
“Wataendelea kulalamika hivi hivi hadi ile Katiba ya Warioba itakaporudi na kumpunguzia Rais madaraka kama ilivyokuwa imetamka,” alisema mchungaji huyo.
Chanzo:  Gazeti la Mtanzania
0 comments

Hiki ndicho kimewang'oa Wakurugenzi na Mameneja NSSF


Nyumba za Mradi wa Kijichi

UBADHIRIFU wa fedha na ukiukwaji wa taratibu na sheria katika usimamizi wa miradi kadhaa ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), vimeelezwa kuwa miongoni mwa sababu za kusimamishwa kazi wakurugenzi sita na mameneja watano wa shirika hilo.
Vigogo hao walisimamishwa kazi juzi na Bodi ya Wadhamni ya NSSF inayoongozwa na mwenyekiti wake, Profesa Samwel Wangwe, kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya ofisi na kutofuata kanuni, sheria na taratibu katika uwekezaji, usimamizi wa miradi, ununuzi wa ardhi na ajira katika shirika hilo.
Waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi, Yacoub Kidula, Mkurugenzi wa Fedha, Ludovick Mrosso, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Chiku Matessa na  Mkurugenzi wa Udhibiti, Hadhra na Majanga, Said Shemliwa.
Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Hesabu za Ndani, Pauline Mtunda na Mkurugenzi wa Uendeshaji, Cresentius Magori.
Mameneja waliosimamishwa ni Meneja Utawala, Amina Abdallah, Meneja wa Uwekezaji, Abdallah Mseli na Meneja wa Miradi, John Msemo.
Wengine ni Mhasibu Mkuu, John Davis Kalanje, Meneja Kiongozi Mkoa wa Temeke, Wakili Chedrick Komba na Meneja Miradi, John Ndazi.
Inaelezwa kuwa baadhi ya ubadhirifu huo ulifanywa kupitia miradi ya usimamizi wa nyumba za kuuza zilizopo Mtoni Kijichi, Dar es Salaam, unaokadiriwa kufikia Sh bilioni 137.7.
Katika ripoti ya mwaka ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu ukaguzi wa mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha 2014/2015, imebainika kuwa ulikuwapo ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika miradi hiyo.
Taarifa hiyo ya CAG inaeleza katika ukurasa wa 165 na 166 kuwa Juni 30 mwaka 2015, Sh bilioni 79 za shirika hilo  zilitumika katika ujenzi wa nyumba hizo ambazo ziliamuriwa kuuzwa ndani.
Uamuzi huo ulitolewa badala ya kufuata maelekezo ya wasimamizi kwa kutumia benki au makampuni ya mikopo kama ilivyoelekezwa katika kanuni namba 13 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na mwongozo wa uwekezaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika maoni yake kuhusu mradi huo, ofisi ya CAG iliishauri menejimenti ya NSSF kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa na wasimamizi wake.
“Kitendo chochote cha kutofuata maagizo kinatakiwa kuwasilishwa kwa maandishi kwa mdhibiti wa sekta na kukubaliana muda uliopangwa kwa ajili ya kufuatwa,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Ukiukwaji mwingine wa sheria na taratibu unaotajwa kufanywa na vigogo hao, ni ununuzi wa ardhi bila ushindani kutoka kwa muuzaji mmoja, kwa gharama ya Sh bilioni 15.16.
Taarifa hiyo ya CAG inaeleza kuwa NSSF ilipanga bajeti ya Sh bilioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa kiwanja kupitia zabuni za ushindani.
“Hata hivyo, ilitumia chanzo kimoja katika ununuzi wa kiwanja kilichogharimu Sh bilioni 15.16. Nimegundua kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma haikujulishwa, kinyume cha kanuni namba 87 ya mwaka 2013 ya mamlaka hiyo inayohitaji kuwasilishwa taarifa za mkataba wa tuzo kwake, ndani ya siku saba kuhusu mchakato wa ununuzi endapo chanzo kimoja kilitumika,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya CAG.
CAG aliishauri menejimenti ya NSSF kuzingatia mpango wake wa bajeti na kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013, kuhakikisha ununuzi unafanyika katika ushindani ili kupata huduma kwa bei nafuu.
Kutokana na hali hiyo, katika ripoti hiyo ya ukaguzi, CAG alieleza namna NSSF lilivyoingia ubia na Kampuni ya Azimio Housing Estate kuanzisha kampuni maalumu kwa jina la Hifadhi Bulders Limited.
Katika mkataba huo, Azimio Housing Estate inatakiwa kuendeleza ekari 20,000 za ardhi zilizopo Kigamboni ambapo kwa hatua ya awamu itaaanza na ekari 300.
“Katika ubia huu, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii linamiliki asilimia 45 ya hisa wakati Azimio Housing Estate inamiliki asilimia 55. Jumla ya gharama za mradi ni dola za Marekani milioni 653.3.44.
“Ukaguzi wa hatimiliki umeonyesha kuwa Azimio Housing Estate inamiliki viwanja viwili, kiwanja chenye hatimiliki namba 81828 chenye ukubwa wa hekta 1.98 na chenye hatimiliki namba 105091 chenye ukubwa wa hekta 114.11 ambavyo vyote vinapatikana katika eneo la Rasi Dege,” ilieleza taarifa ya CAG.
Pamoja na hali hiyo, CAG alisema kuwa hajaweza kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo Azimio iliahidi kutoa kama uchangiaji wa mtaji hali ambayo NSSF ililipa asilimia 20 ya fedha kama mtaji ambazo zilikuwa kwenye hatari ya kupotea.
Licha ya kuibuliwa kwa hili, CAG alieleza kuwa Menejimenti ya NSSF ina udhaifu katika mifumo ya kifedha na kiuhasibu. Kwamba wana mfumo mkuu wa usimamizi wa rasilimali ambao unaweza kuunganishwa na mfumo wa usimamizi wa fedha ambao unakosa moduli ya uhasibu kwa ajili ya kuhifadhi taarifa za kifedha.

DENI LA BIL 723.22
Katika taarifa hiyo ya CAG, inaelezwa kuwa NSSF iliikopesha Serikali katika miradi yake mbalimbali, lakini hata hivyo imekuwa hailipi madeni yake kwa muda mrefu.
Kwamba hali hiyo imekuwa ikisababisha kuongezeka kwa limbikizo la riba na adhabu hadi kufikia asilimia 39 ya salio la Sh bilioni 729.22 kufikia Juni 2014.

WAFANYAKAZI NA MADENI
Shirika hilo lina utaratibu wa ndani wa kutoa mikopo kwa wafanyakazi wake, na ukaguzi umeonyesha kiasi cha Sh milioni 827.98 bado kinadaiwa kwa wafanyakazi ambao si waajiriwa tena wa NSSF.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais John Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau na kumteua kuwa balozi ingawa hadi sasa hajapangiwa nchi ya kwenda.
Vilevile, mwanzoni mwa Machi mwaka huu, mrithi wa Dk. Dau, Dk. Carine Wangwe ambaye aliteuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, uteuzi wake ulitenguliwa na Ofisi ya Rais Ikulu katika kile kilichoelezwa kuwa ulikiuka taratibu.

KUHOJIWA TAKUKURU
Wakati huohuo, taarifa zilizoifikia MTANZANIA jana, zilisema vigogo hao wameanza kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu suala hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema yuko nje ya ofisi na akashauri atafutwe msemaji wa taasisi hiyo, Mussa Misalaba.
Hata hivyo, Misalaba alipoulizwa, alisema hana taarifa na jambo hilo kwa sababu hakuwa ofisini.
Chanzo: Gazeti la Mtanzania
0 comments

Sendeka: Uchaguzi wa viongozi CCM si wa kupokezana.

Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni sio wa kupokezana vijiti, kwa sababu nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti unapofika wakati wa uchaguzi haziombwi, bali yanapendekezwa majina ya watu wanaofaa kushika nyadhifa hizo na kuteuliwa.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka na kusema kama atachaguliwa, Rais Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa CCM wa tano baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.
“Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wawili unapofikia wakati wa uchaguzi nafasi hizi haziombwi isipokuwa Kamati Kuu inafikiria na kupendekeza majina na kuyawasilisha kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo humteua,” amesema Sendeka.
Amesema baada ya hapo Mkutano Mkuu wa Taifa unamchagua kwa kumpigia kura na kuongeza kuwa wanaopendekezwa hawajazi fomu za kugombea nafasi hizo na katika mchakato huo kinachofanyika si kupokezana kijiti, kama wengi wanavyopenda kuita, bali ni uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa CCM.
“Katika uchaguzi huo itapigwa kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’ ili kupata mwenyekiti na lazima apate nusu ya kura na akipata chini ya nusu mapendekezo yataanza upya,” ameongeza Sendeka.
Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wajumbe 2,456 na mpaka sasa wamekodi hoteli 306 ambazo zitawalaza zaidi ya watu 3,331 mjini Dodoma.
Viongozi watakaojiuzulu ili kupisha Dkt. Magufuli kupanga safu yake mpya ya uongozi ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Manaibu Katibu Wakuu wawili na watendaji wengine.
Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Katibu wa Oganaizesheni, Katibu wa Siasa na Uhusiano ya Kimataifa, Katibu wa Uchumi na Fedha na wa Itikadi na Uenezi.
“Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana atakabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa chama kupisha Rais Magufuli aweze kuunda safu yake ya watu atakaofanya nao kazi,” amesema Sendeka na kuongeza kuwa anaamini Magufuli ataunda safu nzuri itakayoleta mabadiliko.
Chanzo: Hivisasa blog
0 comments

Jaji Ramadhan aungana na akina Lowassa, Sumaye na Mwandosya




JAJI Mkuu mstaafu  wa Tanzania, Augustino Ramadhani amesema utaratibu uliotumiwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) wa kukata majina yao katika uteuzi wa urais haukuwa wa haki.
Amesema hakupata nafasi ya jina lake kuchekechwa katika uteuzi huo, bali kalamu ilipita na majina yao yakakatwa.

Amesema amepanga kwenda kuonana na uongozi wa juu hivi karibuni, kutokana na kile alichosema hakubaliani na baadhi mambo ndani ya chama hicho tawala,

Jaji Ramadhani ambaye alikuwa miongoni mwa wagombea waliosaka tiketi ya urais kupitia CCM, sasa anaungana na waliokuwa wagombea wenzake kukosoa mchakato huo wa ndani ya chama.

Jaji Ramadhani anaungana na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa  Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na Profesa Mark Mwandosya ambao walitoka hadharani na kueleza kutoridhishwa na mchakato huo.

Jaji Ramadhani ambaye hivi sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika ofisini kwake jijini Arusha juzi.

“Sikupata hata nafasi ya jina langu kuchekechwa kwenye mchakato wa uteuzi wa urais ndani ya CCM… kalamu ilipitia tu majina yetu yakaondolewa na tulitumia busara mno kukaa kimya,”alisema Jaji Ramadhani.

Sababu za kuchukua fomu 

Akizungumzia sababu zilizomsukuma achukue fomu ya kugombea urais, Jaji Ramadhan alisema alitegemea  rais wa awamu tano angetoka Zanzibar, baada ya Bara kuongoza kwa awamu mbili mfululizo.
Alisema sababu nyingine ni kutokana na dhuluma nyingi na haki za binadamu kuvunjwa, hivyo aliamini angeleta mabadiliko.

“Niliamini sasa ni zamu ya Zanzibar baada ya Bara kuongoza kwa awamu mbili. Kuna siku nilikutana na Kingunge Ngombale Mwiru kwenye mkutano fulani, nikamwambia kuhusu idadi ya Serikali, yeye anasema kuwa na serikali tatu inavunja Muungano, nikamwambia je kuwa na marais mara tatu mfululizo kutoka upande mmoja haina athari…akanijibu ‘you have a point’ kwa hiyo ndiyo hivyo.

Alipoulizwa kuhusiana na namna alivyoshtua watu wengi pale alipochukua fomu, Jaji Ramadhan alisema hakushtua bali baadhi ya wanasiasa walikuwa wakieneza propaganda chafu, baada ya kuona rekodi yake haina shaka katika uongozi.

“Watanzania hawakushtushwa, wengi walifurahi wakaona sasa wamepata mtu kwa sababu wanajua rekodi yangu katika uongozi, wachache wa kisiasa ndio walikuwa wanaeneza propaganda chafu kwa sababu wananiogopa.

“Miongoni mwao ni mwanahabari mmoja (anamtaja jina)naye alikuwa akiandika habari za kunichafua kuwa inakuwaje jaji awe ndani ya chama cha siasa na agombee urais, lakini nilimpigia nikamwonya,”alisema Jaji Ramadhani.

Kada CCM

Jaji Ramadhan ambaye pia ni askari mstaafu wa  Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye cheo cha  Brigedia Jenerali, alisema tangu alipostaafu ujaji alikuwa mwanachama wa CCM hadi sasa.

“Mimi ni mwanachama wa CCM,  kuna mambo ambayo sikubaliani nayo na hayako sawasawa ndani ya chama, nimepanga kwenda kuonana na uongozi wa chama kuwashauri,”alisema.
 
Amkwepa Rais Magufuli

Alipotakiwa na gazeti hili kutoa maoni yake kuhusiana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, Jaji Ramadhan alisema anamtakia kila heri.

BUNGE LA 11

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa Bunge la 11, Jaji Ramadhani alieleza kusikitishwa kwake kwa kitendo cha polisi kuingia ndani ya Bunge na kuwatoa nje wabunge.

“Kwanza sijafuatilia sana… kitendo cha polisi kuingia ndani ya Bunge si sawa kabisa. Mimi pamoja na ujaji wangu kuna mipaka ya kuingia bungeni, hatuingii ovyo ovyo.

“Kuna askari wa Bunge pale, kwanini polisi waingie bungeni…huku ni kuvunja heshima za taasisi zetu si sawa kabisa,”alisema.

Chanzo: Gazeti la MTANZANIA
1 comments

Miss albino Mwanza Apatikana


HATIMAYE shindano la kumsaka mrembo  alibino jijini Mwanza limefikia tamati baada ya ZAWADI Dotto (17) kuibuka kidedea na kutawazwa kuwa mshindi katika shindano hilo baada ya kuwagaragaza wapinzani wake sita.

Shindano hilo lililofanyika juzi usiku jijini hapa huku likiwakutanisha
wasichana saba wenye ualbino ili kumpata mshindi
atakaye wakilisha Mkoa kitaifa.

Warembo hao Hajra Sadru, Furaha Elias, Zabibu Abdalah, Anthonia
Mathias,Pendo Faustine na Asteria Christopher walionyesha madaha na ubunifu jukwaani
wakisaka nafasi hiyo.
Hata hivyo walioingia tatu bora katika mpambano huo ni Zawadi Dotto, Furaha Elias
na Hajra Sadru,ambapo Dotto aliweza kung’ara zaidi na kuwaacha wawili
hao.



Mara Baada ya Zawadi Dotto kutangazwa mshindi, alisema kuwa hakuamini
kama angeweza kushika taji hilo na kuahidi kuwa atahakikisha
anasimamia haki za watu wenye ulemavu wa ngozi.

Pia aliwashauri walemavu wa ngozi kujitokeza kugombea nafasi za
mbalimbali za uongozi ili kuleta usawa kwenye jamii na kuitaka
serikali kutoa fursa kwa maalbino.

“Kwakeli sikutarajia kama ningeweza kushinda taji hili,kwasababu wote
umewaona walivyo safi,mimi nakiri kuwa ni kudra za Mungu labda nitapambana
kupigania haki za watu wa Albino”alisema Dotto

Mlimbwende huyo aliweza kujinyakulia zawadi ya Simu aina ya Solar
5,kitita cha Sh 100,000 na Godoro,huku mshindi wa pili Hajra Furaha simu,godoro na Sh 80,000  na watatu simu,godoro na Sh 50,000.
Mwisho
2 comments

JK ateuliwa mjumbe AU




Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete, ameteuliwa kuwa mjumbe mpya wa umoja wa Afrika AU kwenda nchini libya akichukua nafasi ya Mohamed Dileita aliyeshika nafasi hiyo tangu mwaka 2014.

Uteuzi huo uliofanywa na Umoja wa Afrika katika kikao chake kilichofanyika jijini Addis Ababa nchini Ethopia kimeleza uteuzi huo ni   sehemu ya juhudi za umoja huo kuhikisha usalama unarudi nchini libya.

Kamishina wa Amani na usalama wa AU,Smail Chergui jana alitangaza uteuzi huo alipokuwa anatoa muhtasari wa majadiliano na makubaliano ya kikao hicho kilichiwakutanisha viongozi wa ngazi za juu wa nchi wanachama.

Chanzo: Hivi sasa
0 comments
 
Support : GUDMUSICS BLOG | Gm Template | Gm Template
Copyright © 2015. NGOWI HABARII - All Rights Reserved
Template Created by 0756494700 Published by GM Template
Proudly powered by gudmusics blog