vote

Waathirika wa mafuriko Buchosa Wasaidiwa

 
Mafuriko

KAYA 33 zilizopata maafa ya kuharibiwa makazi na mali mbalimbali
kutokana na kimbunga kilichoambatana na mvua katika Jimbo la Busega
wilayani Sengerema, zimepata msaada wa chakula na sabuni wenye thamani
ya Sh milioni nne kutoka kwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eston
Kasika  (Jowa).

Tukio hilo la maafa lililosababisha watu 189 kukosa makazi baada ya
nyumba walizokuwa wanaishi kuezuliwa, lilitokea Aprili 13, mwaka huu
saa sita mchana katika vijiji vya Mbugani na Bulyaheke katani
Bulyaheke, ambapo wawananchi kadhaa walipata majeraha madogo madogo.

Msaada huo unahusisha kilo 1,320 za unga wa mahindi, maharage kilo
360, mchele kilo 460, mafuta ya kula lita 40, sukari kilo 66, katoni
mbili za chumvi, katoni 40 za maji ya kunywa, katoni sita za sabuni za
kuogea na kufulia.

Akikabidhi msaada huo kwa viongozi wa vijiji na kata husika ambao nao
waliugawa kwa waathirika hao katika ofisi ya kata hiyo jana, Kasika
alisema amejitokeza kutoa msaada huo ili kuwapunguzia wananchi hao
tatizo la ukosefu wa chakula na sabuni za kuogea na kufulia mavazi.

Hata hivyo, kada huyo ambaye anatajwa kuwani ubunge wa Buchosa mwaka
huu, alisema ametoa msaada huo siyo kwa kushindana na yeyote, bali kwa
nia ya kuwadaidia waathirika hao na kuhamasisha watu wengine
kujitokeza kuwasaidia kwa hali na mali.

“Ninatoa msaada huu kuwasaidia ndugu zangu hawa nikiwa kama ndugu yao
na mkazi wa jimbo hili [Buchosa], sifanyi hivi kwa kushindana na mtu,
hiki ni kilio cha nyumbani,” alisisitiza Kasika.

Alitumia nafasi hiyo pia kupongeza jitihada za hali na mali
zilizofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Zainabu Tarak, viongozi
wa kata, vijiji na vitongoji husika katika kuwasaidia waathirika wa
maafa hayo.

Diwani wa kata ya Bulyaheke, Bageti Nyuki Ngele na Ofisa Mtendaji wa
kata hiyo, Mabula Enock, walitoa wito kwa watu wengine kujitokeza
kuwapatia waathirika hao misaada ya hali na mali ikiwa ni pamoja na
kuwawezesha kupata makazi kwani kwa sasa wamepewa hifadhi ya muda
kwenye jengo la ofisi ya kata hiyo.

Walisema mbali ya chakula, waathirika hao wanahitaji misaada ya
blanketi, vyandarua na dawa kujikinga na magonjwa mbalimbali.


Share this article :

Post a Comment

 
Support : GUDMUSICS BLOG | Gm Template | Gm Template
Copyright © 2015. NGOWI HABARII - All Rights Reserved
Template Created by 0756494700 Published by GM Template
Proudly powered by gudmusics blog