skip to main |
skip to sidebar
Geita
KATIBU Msaidizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita
amevuliwa madaraka na ofisi yake kufungwa baada ya kutuhumiwa kujihusisha na
ubadhirifu wa Sh milioni sita za chama hicho.
Kwa muda mrefu, katibu huyo, Patrick Kusaga, amekuwa akidaiwa
kulindwa na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wilayani hapa wanaowania ubunge
wa jimbo la Geita.
Katibu huyo alikumbwa na adhabu hiyo baada ya kikao kamati ya
siasa ya CCM wilayani kufikia uamuzi huo mjini hapa, juzi.
Kusaga anatuhumiwa 'kutafuna' mamilioni hayo ya fedha yaliyotokana
na kodi za pango.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mwenezi wa CCM wilaya
hapa, Jonathan Masele, alisema mbali ya kufanya ubadhirifu huo, Kusaga pia
amekuwa akionyesha dharau kwa viongozi wenzake.
Masele aliongeza kuwa kamati ya siasa ya wilaya imekuwa ikimwita
mara kwa mara ili kuzungumzia tuhuma zake, lakini amekuwa akiwatolea majibu ya
kejeli, jambo ambalo limesababisha kumng'oa madarakani.
“Tumefikia maamuzi haya kutokana na katibu huyu msaidizi kujiona
yeye ni zaidi ya wenzake na kujipa madaraka makubwa, amehusika na upotevu wa
shilingi milioni sita za kodi. Kutokana na hayo, kamati ya siasa ya wilaya
imemwita mara kadhaa, lakini ameshindwa kutii wito na amekuwa akitutolea lugha
za kejeli kuwa sisi hatuwezi kumfanya chochote kwa kuwa anawakubwa wanaomlinda,”
alisema na kuongeza:
“Kamati ya siasa ya wilaya hatumtaki, labda mkoa au makao makuu
wampeleke wanakojua wao, lakini hapa hatumhitaji, anasababisha chama kiyumbe na
anaweza kusababisha tulikose hili jimbo la Geita, tumeamua kufunga na ofisi
yake hapa, tunasubiri kuletewa mtu mwingine, huyu hafai kabisa kuwa hata balozi
kwa ufisadi wake. Kadi za CCM tunaziuza shilingi 300, lakini yeye anaziuza
shilingi 540 kinyume na utaratibu.”
Hata hivyo, Kusaga alipoulizwa na gazeti hili alisema hajui lolote
kuhusu suala hilo na kwamba alikuwa njiani akitokea wilayani Butiama, Mara
kwenye msiba wa mtoto wa Mwalimu Julius Nyerere, John Nyerere.
“Hizo tuhuma mimi sizijui na sijaitwa na tunapoongea nipo Mwanza
natoka Butiama kwenye msiba wa mtoto wa Mwalimu Nyerere," alisema Kusaga.
Taarifa kutoka ofisi ya CCM wilayani hapa pia zilidokeza kuwa
huenda Katibu wa wilaya naye akatimuliwa kutokana na tuhumza za kushirikiana na
huyo msaidizi wake katika matumizi mabaya ya madaraka.
''Nikuambie ni muda mrefu hawa watu wamekuwa wanatusumbua sana,
ukiwaita hawaji, lakini katika kuhakikisha tunafanya vizuri katika uchaguzi ujao
ni vyema hawa watu waondoke tuletewe wengine, vinginevyo watatuharibia uchaguzi
mkuu," alisema mmoja wa makada wa CCM wilayani hapa aliyeomba kutotajwa
jina.
Post a Comment