Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. |
Rais Jakaya Kikwete ametaja sifa za mrithi wake kufuatia hatua za mwisho kumaliza utawala wake uliodumu kwa muda wa miaka kumi.
Akibainisha sifa za mtu anayetakiwa kuteuliwa na kamati kuu mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM amesema kamati hiyo haina budi kumchagua mgombea urais anayekubalika ndani na nje ya chama hicho.
Kikwete amesema hayo wakati akifungua kikao cha Halmashauri Kuu kwenye ukumbi wa ofisi ya makao makuu ya chama hicho mkoani Dodoma
“Watanzania wote bila kujali itikadi zao wanaitazamia na kuitumainia CCM kutoa uongozi ulio bora kwa nchi yetu. Hali hii inathibitisha uleusemi wa Baba wa Taifa kwamba Rais anaweza kutoka chama chochote lakini rais bora atatoka CCM,” alisema.
Ameongeza kuwa wakimpata mtu ambaye CCM inampenda, lakini wananchi hawatampenda, chama hicho kitaumia, dhana ya kuwa wakichagua mtu yoyete mradi katoka CCM, watakuja kukiona cha mtema kuni.
Aidha, kamati kuu CCM ipo katika mchakato wa kumpata mgombea mpya baada ya Rais Kikwete kumaliza muda wake wa vipindi viwili vinavyokubalika kikatiba, huku kukiwa na ongezeko kubwa la nguvu ya upinzani.
Hata hivyo Kamati Kuu ya CCM imewaachia huru makada wake sita waliotumikia adhabu ya miezi 17 ya kuzuiwa kujishughulisha na shughuli za uchaguzi baada ya kubainika kukiuka sheria za uchaguzi za chama hicho kutokana na kuanza kampeni mapema.
Makada waliangukiwa na adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Uchaguzi mkuu wa Rais pamoja na wabunge mwaka huu unatarajia kufanyika wiki mwisho ya mwezi oktoba kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Chanzo: Hivi Sasa
Post a Comment