Uandikishaji Wakimbizi mkoani Kigoma kutoka nchini Burundi. |
Raia wa Burundi wameendelea kuingia nchini Tanzania kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo ambapo hadi kufikia tarehe 03 Mei, 2015 raia wa Burundi waliongia nchini kuomba hifadhi walikuwa 1,852.
Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi ya Tanzania Isaac J. Nantanga amesema kwamba raia hao wa Burundi waliingia nchini kupitia vijiji mbalimbali vya mkoa wa Kigoma.
Vijiji hivyo ni pamoja na kijiji cha Kigaye, Sekeoya na Kakonko. Vingine ni Kosovo, Kagunga na Kibuye, huku wengine wakiwa wamepitia katika Kituo cha Uhamiaji cha Manyovu kilichopo mkoani Kigoma.
Baada ya kufanyiwa mahojiano ya kina katika kituo maalumu kilichopo mjini Kigoma, 1,252 kati yao wamehamishiwa katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko wilayani Kasulu Mkoani Kigoma
Akizungumzia hali ya ulinzi na usalama katika maeneo wanapoingilia amebainisha kuwa hali ni shwari na hadi sasa hakuna matukio yoyote ya uhalifu yalitolewa taarifa.
Wananchi wa Burundi wamelazimika kuikimbia nchi yao kufuatia kuibuka mgogoro uliosababishwa na Rais Nkurunziza kutaka kuwania tena urais kwa mara nyingine kinyume na katiba ya nchi hiyo.
Chanzo: Hivi Sasa
Post a Comment