Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa |
RAIS Mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ameitaka Tanzania kuacha kutegemea misaada mingi kutoka nje ya nchi na badala yake tuwe na nia ya dhati ya kukuza uchumi wetu.
Akizungumza wakati wa ibada ya kuadhimisha miaka 19 ya
uinjilishaji wa RedioMaria iliyoambatana na harambee ya kuchangia kituo
hicho juzi, Mkapa alisema imefika wakati Tanzania tusitegemee misaada
kutoka mataifa ya ulaya na tujitahidi kujiwezesha yaliyo ndani ya uwezo
wetu kwani tukiamua tunaweza kujitegemea.
Mkapa alisema kwa sasa hata misaada ya maendeleo inayotoka
mataifa ya ulaya imepungua na ukiwauliza wanasema na wao wana shida
kubwa sana kwa kweli tusitegemee misaada kutoka nje.
“Wahisani huko nje wamechoka na naweza kuwathibitishia
hilo, katika safari zangu huko nje za kujaribu kutetea maslahi ya
Afrika nakuta kweli wamechoka .
“Ulaya ambayo ilikuja ikatumia rasimali na watu wetu kwa
mazingira ya utumwa sasa wangekuwa tayari kuwapokea watu wetu maelfu kwa
maelfu huko nyuma walichukua mamilioni lakini tukijituma kwenda kwa
maelfu wamechoka hawawezi kutuhudumia,” alisema Mkapa.
Hata hivyo amewataka wanasiasa wanaostaafu kustaafu
kwelikweli na kuacha kuendelea kujiingiza katika siasa ili kuimarisha
dhana ya wanasiasa kustaafu hapa nchini.
“Ukistaafu siasa staafu kweli kweli na nilipoambiwa sehemu
nyingine niliwaambia mimi ni mstaafu na maana ya kustaafu ni kufunga
mdomo,” alisema Mkapa.
Pia amewataka watanzania kuepuka kishawishi cha kujiingiza
katika makundi ambayo yanaweza kuiletea nchi athari hasa katika kipindi
hiki tunachoelekea katika uchaguzi mkuu.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, Rais wa Redio Maria
Tanzania, Julius Humphrey, alisema kwa sasa wameamua kujikwamua na
kuacha kuomba misaada maitaifa ya ulaya kama ilivyokuawa awali na kwa
miezi sita sasa wamefanikiwa.
“Tangu mwezi Januari mwaka huu tumekua tukijiendesha kwa
fedha zetu na kwa michango ya marafiki wema wa Redio Maria na
tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa na tunaamini kwa kipindi kilichobaki
tutaweza pia,” alisema Humphrey.
Humphrey ametoa wito kwa watanzania na wadau wote wa Redio
Mario kusali bila kuchoka ili tuweze kupata viongozi bora mfano wa nabii
Musa watakaoweza kutuvusha katika changamoto mbalimbali zinazo ikabili
nchi.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza,
Mwashamu Askofu Yuda Rwaichi, amewataka wakristo wote kuendele kuliombea
Taifa ili tuendelee kufurahia amani iliopo has katika kipindi hiki
tunachoelekea uchaguzi mkuu.
Post a Comment