Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe. |
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameanza ziara ya siku sita kwenye mikoa ya Tabora, Shinyanga, Mwanza na Kagera.
Aidha, ziara hiyo inalenga mwendelezo wa uzinduzi wa programu ya FTP maalum kwa ajili ya mafunzo ya uzalendo kwa vijana, shughuli ambayo amekuwa akiifanya tangu Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, ilisema ziara hiyo aliianza jana katika Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora zitaambatana na mikutano ya hadhara wilayani Bariadi, Shinyanga kabla ya kwenda wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza.
Programu hiyo itazinduliwa pia Bukoba Mjini kisha Kyerwa na kwamba katika maeneo yote wamelialika Jeshi la Polisi kutoa elimu ya ulinzi shirikishi na polisi jamii.
Makene ameongeza pia, wameialika Taasisi ya Kupambana na kuzuia Rushwa (Takukuru) ili kutoa elimu ya kupambana na kuzuia rushwa hasa wakati wa uchaguzi.
Amebainisha kuwa viongozi wengine wajuu wa chama hicho wataendelea na programu ya uzinduzi wa mafunzo ya kukiandaa chama kushinda dola na kuiongoza serikali, kwenye mikoa ya Tanga, Shinyanga na Mbeya.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti Taifa Bara, Prof. Abdallah Safari, atakuwa Korogwe Mjini na kuzindua mafunzo hayo kwa viongozi wa Korogwe mjini na vijijini kisha kufanya mkutano wa hadhara Korogwe mjini.
Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika, atazindua mafunzo wilayani Bariadi na pia atakuwa na mkutano wa hadhara Bariadi na Maswa.
Post a Comment