Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad. |
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ameishutumu vikali Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa madai kuwa iliandikisha na kuruhusu wapigakura wasiostahili zaidi ya 10,000 kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, wakiwamo marehemu 8,507.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana amesema wapigakura hao wasiostahili, bado wapo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura la Zanzibar hadi hivi sasa.
Amesema licha ya baadhi ya watu hao kuwa marehemu na wengine wasiokuwa na sifa, bado hawajafutwa kwenye daftari hilo tangu 2010 na majina yao yatatumika kupiga kura mwaka huu. ZEC iliandikisha katika daftari hilo wapigakura wenye umri chini ya miaka 18, ambao si wakazi katika maeneo waliojiandikisha na waliotumia majina na picha ambazo siyo zao.
Aidha, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, amesema hayo yote yamebainika kufuatia utafiti wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Zanzibar uliofanywa kati ya Agosti 2014 hadi Machi 2015.
Utafiti huo unaonyesha kuwa kuna zaidi ya watu 10,000 ambao waliandikishwa kinyume na sheria na kwamba walipiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Akitoa mfano huku akirejea utafiti huo, Maalim Seif alidai kwamba katika Jimbo la Donge, ZEC iliandikisha watoto 463 ambao hawajafikisha umri wa miaka 18 na kwamba walipiga kura.
Hata hivyo amesema kwamba alishindwa kuibua suala hilo mara baada ya uchaguzi kufuatia kukosekana ushahidi, hivyo basi sasa anao ushihidi wa kutosha kuhusiana na rafu hizo.
Katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2010, Zanzibar mgombea urais wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein alipata kura 179,809 sawa na asilimia 50.1 wakati Maalim Seif wa CUF alipata kura 176,338 sawa na asilimia 49.1.
Chanzo: Hivi Sasa
Post a Comment