Wizara ya Afya yatoa Ufafanuzi kuibuka kwa Kipindupindu Dar, Morogoro
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa ufafanuzi juu ya hali ya ugonjwa wa kipindupindu katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro na kuwatahadharisha wananchi kufuata kanuni za Afya, kama vile kunawa mikono na sabuni baada ya kutoka chooni na kabla ya kula chakula pamoja na kunywa maji yaliyo chemshwa au kutibiwa na dawa ya aina ya klorini.
Katika taarifa yake Wizara ya Afya imeeleza kuwa Ugonjwa wa kipindupindu katika mkoa wa Dar es Salam umeripotiwa katika Manispaa ya Kinondoni kuanzia tarehe 15 Agost, 2015 ambapo tangu ugonjwa uanze hadi kufikia jana Agost 20 idadi ya wagonjwa walioripotiwa ni 56 na vifo vya watu watatu.
Wagonjwa walioathirika wanatokea maeneo ya Tandale, Mikocheni, Saranga, Kijitonyama, Makumbusho, Ubungo, Kigogo, Manzese, Kawe na Kimara katika Manispaa ya Kinondoni.
Wakati huohuo Mkoani Morogoro wagonjwa nane wameripotiwa na kifo cha mtu mmoja na wanatokea katika maeneo ya Kilakala na Mzinga Juu.
Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaoambukizwa kwa kula chakula au kinywaji chenye vimelea vya “Vibrio cholera” ambavyo ndivyo husababisha ugonjwa wa kipindupindu. Vimelea hivi hupatikana kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote kimechafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.
Aidha taarifa hiyo imefafanua Dalili kuu za ugonjwa huo ni pamoja na kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji meupe kama maji ya mchele na kunaweza kuambatana kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu.
Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapataa huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji.
Zimetajwa hatua ziizochukuliwa ni pamoja na Kufungua kambi za wagonjwa wa kipindupindu katika Manispaa zote tatu za Dar es Salaam ambapo kwa Kinondoni kambi ipo Mburahati, Ilala kambi ipo kituo cha afya Buguruni na Temeke katika Hosipitali ya Temeke,Kutoa dawa, vifaa vya maabara na vifaa kinga, Kupima vipimo vya maabara na kubaini aina ya vimelea vinavyosababisha ugonjwa, Kupeleka timu za watalaam kutoka ngazi ya Mkoa na Taifa kusaidiana na timu za Manispaa husika na Kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya kuhusu ufuatiliaji na matibabu ya ugonjwa wa kipindupindu.
Chanzo: Hivi Sasa
Labels:
habari
Post a Comment