vote
Featured Post Today
print this page
Latest Post

Mazito yaibuka Zanzibar



WATU wasiojulikana wamevamia katika makazi ya watu eneo la Msumbiji mjini Unguja na kuvunja mabanda na msikiti.

Watu hao maarufu kama mazombi, walifanya uhalifu huo usiku wa kuamkia jana, ambapo walivamia eneo hilo wakiwa wamejifunika nyuso zao na soksi maalumu, huku wakiwa na silaha za jadi.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, aliliambia MTANZANIA kuwa watu hao walivamia eneo hilo saa 10 alfajiri.

Alisema watu hao baada ya kufika katika eneo hilo ambalo linadaiwa kukusanya mashabiki wa vyama vya upinzani, walianza kuvunja mabanda ya mafundi seremala.

“Lilikuwa kundi la watu, tena wote ni mazombi, wakiwa na silaha za moto pamoja na zile za kijadi kama mapanga, marungu, mikuki na mashoka.

“Wamefanya uharibifu mkubwa wa mali zetu yakiwamo mabanda ya mbao, msikiti wa mabati wa hapa Msumbiji ambao tumekuwa tukiutumia kama msikiti wa muda wakati  huu wa kisasa ukiendelea kujengwa.

“Vurugu hizi wamefanya zimekuwa kubwa sana na uharibifu, huu kwa kweli ni uonevu wa hali ya juu, wameharibu mabanda karibu yote kama unavyoona  na mengine ya biashara yaliyopo kando ya barabara hadi kufikia eneo la mabati,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazeti kwa kuhofia usalama wake.

MTANZANIA lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Jeshi la Polisi lipo katika uchunguzi.
“Tumepata taarifa za tukio la kuvunja vibanda katika eneo la Msumbiji na Jeshi la Polisi tumeanza msako wa kuwabaini watu waliohusika na tukio hili, ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kamanda Mukadam,

Dk. Shein na Uchaguzi

Katika hatua nyingine, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakina sababu ya kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani hapa.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wana CCM na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kushirki uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Machi 20.

Kauli hiyo imekuja wiki moja baada ya Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), kupitia Kaimu Mwenyekiti wake, Dk. Twaha Taslima, kutangaza chama hicho kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio.

Dk. Shein aliyasema hayo jana mjini Unguja, alipokuwa akihutubia katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, ambapo aliwataka wanachama hao kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akisisitiza amani na utulivu visiwani humo.

“Sisi hatutasusa, tutashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi. Niwaombe nyote wanachama, kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili muichague CCM kwa kura nyingi,” alisema Dk. Shein.

Rais huyo wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, aliwataka wananchi pamoja na viongozi wa CCM kuendelea kushikamana pamoja ili waweze kuleta maendeleo ya kweli ndani ya chama hicho.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewahakikishia wananchi wote kwamba kutakuwa na ulinzi wa hali ya juu katika uchaguzi wa marudio.
“Nawasihi wananchi msiwe na wasiwasi, tutahakikisha ulinzi unaimarishwa ili muweze kupiga kura kwa amani na utulivu,” alisema Balozi Seif.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana,  alimsifu Dk. Shein kwa kuwa kiongozi hodari na ambaye amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Hata hivyo aliwataka wananchama wa CCM kujipanga kwa ajili ya uchaguzi ili waweze kukipatia chama chao ushindi wa kishindo.

“Uchaguzi ni kujipanga, uchaguzi ni mikakati na uchaguzi ni mahesabu, kwahivyo niwaombe na nyinyi mzingatie haya,” alisema Kinana.

Sherehe za maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM hufanyika kila mwaka nchini ambapo kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika mkoani Singida, Februari 6.

Visiwa vya Zanzibar vipo katika sintofahamu ya kisiasa tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, alipotangaza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, wiki iliyopita Baraza Kuu la Uongozi la CUF, kupitia Kaimu Mwenyekiti wake Dk. Taslima, walitangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio.

Kutokana na msimamo huo, mwishoni mwa wiki iliyopita mabalozi wa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) walitoa tamko la kusikitishwa na kitendo cha ZEC kutangaza tarehe ya kurudiwa uchaguzi na kumtaka Rais Dk. John Magufuli kutumia nafasi yake ya uongozi kutatua mtanziko wa kisiasa wa Zanzibar.

Taarifa ya pamoja iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mabalozi hao, pia inamtaka Rais Magufuli kuendeleza wito wake wa kuzitaka pande zote zitafute suluhu kwa amani.

Kutokana na sakata hilo, mabalozi hao wamelaani kitendo hicho wakisema kurudia uchaguzi kwa kigezo kuwa utaratibu ulikiukwa, kinawatia wasiwasi kwa kuwa tume hiyo haikutoa ushahidi wa ukiukwaji huo.

Mabalozi hao walisema katika tamko lao kuwa ZEC imerudia kauli yake ya kuwa uchaguzi ulikiuka taratibu licha ya waangalizi kutoka EU, Jumuiya za Afrika Mashariki, SADC, Marekani na Jumuiya ya Madola kufanya tathmini na kujiridhisha kuwa ulikuwa uchaguzi huru na haki.

Taarifa hiyo iliyotumwa kwa ushirikiano wa mabalozi wa Uholanzi, Norway, Hispania, Italia, Ujerumani, Finland, Ufaransa, Sweden, Uswisi, Uingereza, Ireland na Marekani inasisitiza kuwa kitendo cha upande mmoja kuamua kurudia uchaguzi, kinaweza kuzidisha hofu na taharuki miongoni mwa Wazanzibari.

Chanzo: Gazeti la MTANZANIA
0 comments

Kumbi za harusi, ma-mc kulipa kodi TRA




MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema inafanya utaratibu wa kuhakikisha inawatoza kodi wamiliki wa kumbi za harusi, wapishi na washereheshaji wa sherehe (MC).

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema  wanatarajia kutoza kodi katika sekta hiyo ili kuhakikisha wanaongeza mapato ambayo yatasaidia nchi kupata maendeleo na kuachana na utegemezi kwa wahisani.

Alisema mtu yeyote mwenye vigezo vya kulipa kodi, anatakiwa kujisajili ikiwa ni pamoja na kuchukua namba ya utambulisho (TIN) ambayo itamwezesha kutambulika kirahisi kwenye mfumo wa mamlaka hiyo.

“Kisheria kila mtu au mfanyabiashara anatakiwa kuwa na TIN ambayo itamwezesha kutambulika kirahisi na pia itawasaidia maofisa wetu kuwatambua mahali walipo walipakodi wetu,” alisema Kayombo.

Alisema hivi sasa wapo washereheshaji wanapata kazi na kulipwa kiwango kikubwa cha fedha, lakini hawalipi kodi sambamba na ukodishaji wa kumbi za sherehe.

“Tunajua wapo ma-mc, wapishi wakubwa na hata watu wanakodisha kumbi wanaingiza kiwango kikubwa cha fedha, lakini hawalipi kodi, ni wakati mwafaka nao kuanza kulipa kodi.

“Tunawaomba watupe ushirikiano, hivi sasa unaandaliwa utaratibu mzuri wa kukutana nao kupitia chama chao ili kuwaeleza utaratibu huu mpya ambao utasaidia kujenga nchi yetu na kuwa na maendeleo zaidi,” alisema.

Katika hatua nyingine, mwishoni mwa wiki iliyopita, TRA ilikutana na wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha katika semina ya siku moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafundisha sheria mpya ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)

Source: Gazeti la MTANZANIA
1 comments

Askofu mpya KKKT atahadharisha utumbuaji majipu




ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amemtahadharisha Rais Dk. John Magufuli kuwa kazi ya utumbuaji majipu aliyoanza nayo inapaswa kufanywa kwa kufuata misingi ya haki na busara ili kuepuka watu wasiokuwa waaminifu kutumia mwanya huo kuwaonea wenzao wasiokuwa na hatia.

Akizungumza mbele ya mamia ya waumini wa kanisa hilo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro jana, wakati wa ibada maalumu ya kuingizwa kazini kuwa mkuu wa kanisa hilo, Askofu Shoo alisema kazi ya utumbuaji wa majipu inahitaji hekima na busara ya ki-Mungu na kwamba ifanyike kwa kufuata misingi ya haki pasipo kuwaonea watu wasiokuwa na hatia

“Tuna imani na uongozi wa Serikali ya awamu ya tano na katika kipindi hiki kifupi tumeona juhudi za Serikali katika utumbuaji wa majipu. Utumbuaji huu ufanyike katika misingi ya haki na kwa busara kwani watu wengine wanaweza kutumia mwanya huu kuonea wenzao wasiokuwa na hatia,” alisema.

Mbali na hilo, aliipongeza Serikali ya Dk. Magufuli katika utendaji wake wa kuendelea kuwachukulia hatua watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakijihusisha na ubadhirifu wa mali za umma na ufisadi.

Alisema kwa msingi huo, kanisa hilo bado litaendelea kukemea na kuonya mifumo kandamizi kwa lengo la kujenga maadili mema, upendo, haki na ushirikiano ili kuleta maendeleo ya dhati katika nchi.

Katika hatua nyingine, Askofu Shoo ameonyesha kusikitishwa na vitendo vya ukiukwaji wa maadili na utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya wabunge katika vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.

Kutokana na hali hiyo, Askofu Shoo amewataka wabunge kuendesha vikao vyao kwa kufuata maadili na kuacha mara moja tabia ya utovu wa nidhamu inayojitokeza katika vikao hivyo.
Ibada hiyo ilihudhururiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, dini na Serikali.

Askofu Shoo alisema Bunge ni mhimili ambao haupaswi kuingiliwa na mhimili mwingine, lakini kanisa hilo linasikitishwa na vitendo vya utovu wa nidhamu  vinavyoendelea kufanywa na baadhi ya wabunge.

“Tunahitaji kuona Bunge linajadili vikao vyake kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia. Kanisa linasikitishwa sana na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyoendelea bungeni, tunapenda kuona hoja zinajadiliwa kwa ustaarabu,” alisema.

Askofu Shoo alisema Watanzania wanatarajia kusikia na kuona hoja zinajadiliwa kwa uwazi, hivyo wabunge wana wajibu wa kulinda heshima zao wanapojadili mambo muhimu ya maendeleo na mustakabali wa nchi.

Alisema Bunge ni nyumba ya demokrasia na kamwe haipaswi kulindwa na jeshi.

Wiki iliyopita vurugu kubwa ziliibuka bungeni, baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kutaka kauli ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kuhusu kutorushwa moja kwa moja kwa matangazo ya Bunge ijadiliwe.

Katika vurugu hizo, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kuwalazimisha wabunge wa upinzani kutoka nje.
Baadhi ya wabunge wakiwamo, Susan Kiwanga wa Kilombero na Halima Mdee wa Kawe waliburutwa kwa nguvu na askari hao.

wakati huohuo, Askofu Shoo aliitaka Serikali kuanzisha upya  mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya itakayoheshimu matakwa ya wananchi wote na kuondoa mifumo kandamizi.
Alisema Watanzania wanahitaji Katiba isiyoangalia udini, ukabilia na itikadi za kisasa ambapo kwa namna moja au nyingine, mambo hayo yanaweza  kuligawa taifa na kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani.

Kuhusu suala la elimu, Askofu Shoo aliitaka Serikali kutazama upya sera ya elimu bure na kuboresha shule zake.

Alisema iwapo hatua hiyo itafanyika, hakutakuwa na haja ya kupanga ada elekezi katika shule binafsi kwa kuwa shule za umma zitakuwa na mahitaji yote muhimu yatakayomwezesha mwanafunzi kupata elimu bora.

Aliitaka Serikali kufufua viwanda vilivyokufa kwa lengo la kuzalisha bidhaa zinazotakiwa nchini ili kupunguza kasi ya uagizaji wa bidhaa nje ya nchi, kwani asilimia kubwa zimekuwa feki.

“Serikali ijenge viwanda ili tuzalishe biadhaa zetu wenyewe na kupunguza kasi ya uagizwaji wa bidhaa kutoka nje, jambo hili litasaidia kukuza uchumi wetu na wananchi kuondoka katika hali ya umaskini,” alisema

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Serikali itaendelea kuheshimu michango mbalimbali inayotolewa na taasisi za dini, ikiwamo katika sekta ya elimu na afya.

Alizitaka taasisi za dini kundelea kushirikiana na Serikali katika kuwekeza katika maeneo muhimu kama afya na elimu ili kuboresha utoaji wa huduma katika jamii.

“Napenda kutumia fursa hii kuyashukuru madhehebu ya dini ambayo yamekuwa msitari wa mbele kuisaidia Serikali katika kufikisha huduma hizi za afya karibu zaidi na wananchi. Wito wangu kwa hili, naombeni mjitahidi kutoa huduma hizi kwa gharama nafuu ili wananchi wengi wapate kuzitumia,” alisema.

Naye Askofu Mkuu mstaafu wa kanisa hilo, Dk. Alex Malasusa, akimuingiza kazini Askofu Shoo, alimtaka kuongoza kanisa hilo kwa uaminifu na uadilifu, ikiwa ni pamoja na kuacha kufumbia macho maovu yanayofanyika katika jamii.

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki  Jimbo la Moshi, Mhashamu Isack Amani, aliwataka Watanzania kuwa na moyo wa uzalendo na kuipenda nchi yao, ikiwamo kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

Chanzo: Gazeti la MTANZANIA
0 comments

Chadema: Nape taja gharama za kurusha Bunge 'live' tuchangishe


Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu



Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa tamko kufuatia mpango wa serikali kutangaza kusitisha urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge kuanzia terehe 26.1.2016.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema Chama cha  Chadema kimekosa imani na serikali ya awamu ya tano kwa kuwa na matendo ya kidikteta na kwenda kinyume na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 kwa kutaka kuminya uhuru wa wananchi wa kupata habari.

Akizungumzia matendo hayo amesema ni pamoja na kuzuia Shirikia la Utangazaji la Tanzania(TBC), kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mikutano ya bunge inayoendelea ,kufutwa kwa Gazeti la Mawio pasipo kuwa na sababu za msingi, kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara pamoja na kuunda kamati dhaifu bungeni.

Amesema kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Mnauye ametoa sababu zisizokuwa za msingi akidai kuwa serikali inaepuka gharama za kurusha matangazo hayo moja kwa moja na baadala yake kurekodi vikao hivyo vya bunge kwa  kurushwa saa nne usiku

Amesisitiza kuwa Waziri Nape  hajafanya utafiti na kwamba ikiwa  tatizo lipo kwenye gharama alizotaja chadema ipo tayari kuchangia gharama hizo kwa kuanzisha harambee maalumu pamoja kuwataka chama cha wamiliki wa vyombo vya Habari (Moat) na Baraza la Vyombo vya Habari (MCT) kulisimamia suala hilo.


“Nape ataje gharama hizo tutachangishana mwenye mia moja mia mbili ili wananchi wajue mambo muhimu yanayoendela Bungeni”,alisema Mwalimu.

Akizungumzia Kamati za Bunge amesema serikali imeunda kamati dhaifu bungeni  kwa nia ya kudhoofisha shughuli za utendaji bungeni na maendeleo ya nchi kwa kuwaweka wabunge wageni kwenye kamati muhimu ilhali hawana uwezo kuzisimamia.

Chanzo: Hivi sasa
0 comments

Ugonjwa usiojulikana wavamia Babati mkoani Manyara


Na Wolter John, Babati

Wakazi  wa kijiji cha matufa kitongoji cha Burunge kata ya magugu Wilaya ya Babati mkoani  manyara wameingiwa   hofu kubwa kutokana na kuibuka  kwa ugonjwa ambao haujafahamika mpaka sasa.

Akizungumza na Mwandishi wa Blog hii mwenyekiti wa  kijiji cha  cha burunge  kata ya matufa, Ramadhan Mangi ameeleza kuwa mpaka sasa ugonjwa huo  haujafahamika na  umeua watu wawili wa familia moja huku wengine watano wakiwa bado wanaendelea na matibabu katika kituo cha afya cha Magugu.

Asha Shabani ni mmoja ya waathirika wa ugonjwa huo  na ambaye pia  baba yake amefariki kutokana na ugonjwa huo ameeleza kuwa alianza kujisikia vibaya na kukosa hamu ya kula  na baada ya muda kidogo alianza kutapika,  kuharisha na alipopelekwa hospitali alitibiwa na alipotaka kujua anaugua ugonjwa gani daktari hakuweza kumjibu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji cha Burunge Dismas Baranda  amesema kuwa ugonjwa mpaka sasa una muda wa wiki mbili na kila mgonjwa anapoenda kupima huambiwa ni homa ya matumbo kitu ambacho kinaleta hofu kubwa kutokana na ugonjwa huo kuendelea kusambaa kwa wengine.

Madaktari  wa  kituo cha afya  magugu   wamewaeleza wakazi hao  hawana maabara ya kuweza kupima na hivyo  wamepeleka vipimo katika maabara ya  hospital ya mkoa ya Arusha ya  Mount Meru kwa ajili ya kupata majibu.

Hata hivyo wakazi hao wameshauriwa kutumia maji safi yaliyochemshwa, kula vyakula vya moto,kutoshikana mikono, kuchimba matundu ya vyoo pamoja na kuwapatia vidonge maalum ili kujikinga na ugonjwa huo.
0 comments

Tazama picha za mechi kati ya Stand United na Toto African CCM Kirumba

Mchezaji wa timu ya Stand United, Haruna Chanongo akimtoka Mchezaji wa Toto African juzi katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Timu hizo ziltoka sare ya bao 1-1.



Wachezaji wa timu ya Toto African, Christopher Edward(kulia) na Abdala Seseme wakimkaba mchezaji wa Stand United juzi katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba. Timu hizo ziltoka sare ya bao 1-1.









0 comments

EFG yatoa Mafunzo kwa wanawake wafanyabiashara wa sokoni zaidi ya 100 jijini Mwanza

Baadhi ya wanawake wafanyabiashara wa sokoni wakiwa katika kongamano hilo jijini Mwanza

Baadhi ya wanawake wafanyabiashara wa sokoni wakiiimba kwa furaha katika kongamano hilo jijini Mwanza

Wafanya biashara wa soko la mkuyuni wakijitambulisha katika kongamano hilo

Baadhi ya wanawake walioshiriki katika kongamano hilo jijini hapa






Mkurugenzi Mtendaji wa Equality For Growth(EFG), Jane Magigita akitoa mafunzo kwa wanawake wafanyabiashara walioshiriki kongamano hilo.









ZAIDI ya  wafanyabiashara wanawake 100 mkoani hapa, jana walipatiwa mafunzo ya kukuboresha ushiriki wao, katika shughuli  za kimaendeleo hususa kumwezesha, kutafakari kwa kina tatizo la umasikini na kuweka mikakati thabiti ya kukabiliana nalo.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kongamano la kwanza la wanawake wafanyabiashara sokoni Tanzania lililofanyika Kwenye  ukumbi wa  Mwanza  Hoteli ,  Mkurugenzi wa bodi ya watendaji wa shirika la Equality for Growth (EFG), Emmanuel Tuju alisema, lengo ni kumwezesha mwanamke kutumia zaidi mali, nguvu na jitahada ili kujiletea maendeleo na kulinda haki zao katika umiliki wa mali.

Tuju alisema, sera iliyopo katika sekta isiyo rasmi inawapa wanawake mwongozo wa serikali unaolenga kuwapa  wananchi mwelekeo wa maendeleo unaohakiki  mipango na mikakati  inazingatia usawa wa jinsia kila sekta.

 “Kutokana na hili sisi kama Equality For Growth tumeamua kuleta elimu hii nchi nzima kwa kuanzia mikoa saba ambayo ni Mwanza, Tanga, Shinyanga, Lindi, Mtwara,Mbeya na Dar es salaam, ili  kuhakikisha mfanyabiashara mwanamke anapata haki ya kumili mali zake”.

Mkurungezi mtendaji wa EFG Jane Magigita alisema, wanawake wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwepo na sheria inayosimamia haki zao  kutokana na  mapungufu makubwa yaliyopo, utashi thabiti wa viongozi serikalini pamoja na sera kutumika kisiasa zaidi ya maendeleo.

Alisema ili kuinua maendeleo ya sekta hii, viongozi wanapaswa  kutunga sheria  na kuzisimamia kwa ajili ya  kuboresha miundombinu pamoja na kutoa fursa, haki sawa kwa wananchi walio katika sekta hiyo.

Aidha baadhi ya washiriki wa kongamano hilo ambao pia ni wafanyabiashara wa sokoni walisema, wanakumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo za utozwaji wa ushuru sawa na wafanyabiasha wakubwa.

 Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiasha Soko la Mkuyuni Veneranda Joseph  alisema, Halmashauri imeshindwa kutofautisha wafanyabiashara wadogo na wakubwa wakati wa  kuwatoza ushuru kwani wote  wanalipa kiwango sawa.

 Naye Mwenyekiti wa Soko Kuu mkoani Mwanza Ahmed Nchola alisema, ni vema halmashauri ikatenga   eneo husika kwa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao chini, kwani wengi wao hawaliipi kodi kama wanavyolipa wa maduka na meza.

Hatahivyo biashara ndogondogo huzalisha ajira kwa watu million 2.4 kwa mwaka huku watu 440,000 huingia katika sekta isiyo rasmi  hawa hujumuisha wahitimu wa darasa la saba, waliopunguzwa kazi, wastaafu na wahitimu kutoka vyuoni.

 





0 comments
 
Support : GUDMUSICS BLOG | Gm Template | Gm Template
Copyright © 2015. NGOWI HABARII - All Rights Reserved
Template Created by 0756494700 Published by GM Template
Proudly powered by gudmusics blog